Tamthilia za Kiswahili kama Chombo cha Uhamasishaji kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu: Mifano ya Mwinyi na Manyani ya Adili na Kodi
Keywords:
Malengo ya Maendeleo Endelevu (MME), tamthilia, uchambuzi wa kifasihi, uhamasishaji, uhistoria mpyaAbstract
Azma ya makala hii ni kuchunguza tamthilia za Kiswahili kama chombo cha kuhamasisha jamii kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (MME). MME ni mpango ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015 na umekumbatiwa na serikali, mashirika na wasomi mbalimbali duniani.Utafiti huu ni wa kithamano na unaongozwa na Nadharia ya Uhistoria Mpya iliyoasisiwa na Stephen Greenblatt (1980) na kuendelezwa na Brizee na Tompkins (2012). Muundo wa kiuchambuzi ulitumika kuchunguza jinsi tamthilia teule zinavyoakisi na kuhoji masuala ya kijamii yanayohusiana na MME. Data ilikusanywa kwa mbinu ya unukuzi wa madondoo mahususi kutoka katika tamthilia teule kwa kutumia usampulishaji wa kimaksudi.Tamthilia zilizochaguliwa ni Mwinyi na Manyani ya Adili (Mbogo, 2022) na Kodi (Muhando, 2024) kwa sababu zinaangazia masuala ya MME na ziliandikwa kati ya mwaka 2016 na 2026, yaani kipindi cha utekelezaji wa malengo hayo. Matokeo yamewasilishwa kwa njia ya maelezo ya maandishi.Utafiti umebaini kuwa tamthilia hizi zinahamasisha kwa kiasi kikubwa malengo yafuatayo: L1 (kutokomeza umaskini), L2 (kutokomeza njaa), L5 (usawa wa kijinsia), L8 (ajira na ukuaji wa uchumi), L11 (miji na makazi endelevu) na L16 (amani, haki na taasisi imara). Masuala haya yanajitokeza kupitia wahusika, migogoro na maamuzi yao.Hata hivyo, malengo mengine kama L3 (afya bora), L4 (elimu bora), L6 (maji safi na usafi wa mazingira), L7, L9, L10, L12, L13, L14 na L15 hayajaangaziwa vya kutosha au yamepuuzwa kabisa. Makala hii inapendekeza kwamba waandishi wa tamthilia za Kiswahili wanapaswa kupanua wigo wa maudhui yao kwa kujumuisha kimaksudi malengo yaliyopuuzwa, hasa L3, L4 na L6, ili kuimarisha mchango wa fasihi katika uhamasishaji mpana wa MME.
Downloads
Published
How to Cite
Issue
Section
Copyright (c) 2026 Samuel Sinzore Ogonda

This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.



