Uchunguzi Linganishi wa Dhamira Zinazowasilishwa Kupitia Wahusika wa Kiume Katika Riwaya Teule za Kiswahili
Keywords:
Dhamira, mtazamo, uana, ulinganishi, usawiri, wahusikaAbstract
Makala hii inalinganisha dhamira zilizowasilishwa kupitia wahusika wa kiume katika riwaya teule za Kiswahili zilizoandikwa na wanawake wa Kenya na Tanzania. Tumaini (2006) ya Clara Momanyi, Dago wa Munje (2008) ya Sheila Ryanga, Kipimo cha Mizani (2004) ya Zainabu Burhani, Hiba ya Wivu (1997) ya Zainabu Mwanga. Kuna dhamira za uchapakazi, ndoa, maadili, umuhimu wa elimu, malezi na migogoro ingawa makala hii imejikita katika dhamira mbili ambazo zinalinganishwa katika riwaya teule. Riwaya hizi nne zimeteuliwa kimakusudi kulingana na maudhui mazito yaliyomo katika riwaya hizo kuhusu wanaume. Makala hii imeonesha kuwa nadharia ya ujifunzaji wa kijamii (imejikita kwenye uana) na mwanaume mpya zimekuwa nadharia faafu katika makala hii. Nadharia ya ujifunzaji wa kijamii huona tabia kama kitendo ambacho mtu hujifunza kutoka katika mazingira ambayo ndiyo hupelekea umuhimu wa majukumu ya kiana. Mwisho, makala hii imetumia nadharia ya mwanaume mpya, nadharia inayojaribu kuelezea kwanini baadhi ya wanaume hukaa na wake zao kwa usawa bila tabia za mfumo dume ambazo huashiria kuwepo kwa taasubi ya kiume. Mbinu ya Fasihi Linganishi imetumika kulinganisha usawiri wa wahusika wa kiume katika riwaya teule kupitia dhamira wanazowasilisha. Data iliyotumika katika Makala hii ilitolewa maktabani kwa kusoma tasnifu, makala na vitabu vinavyohusiana na mada. Uwasilishaji wa matokeo umefanyika kwa njia ya maelezo. Matokeo yameonesha kuwa waandishi wa kike wamemsawiri mwanamume kwa mtazamo chanya zaidi kuliko hasi. Kwa hiyo, kulingana na waandishi wa kike wa Tanzania na Kenya wameonesha kuwa mwanamume ni mpya kulingana na mpito wa wakati ambapo mambo mbalimbali ya ugandamizaji wa kijinsia yametupiliwa mbali ili kuleta uwiano wa kiana.
Downloads
Published
How to Cite
Issue
Section
Copyright (c) 2026 Olivia kanwa

This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.